Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Sayyid Mohammad Saeedi, katika khutba za Swala ya Ijumaa ya tarehe 30 January 2026, zilizofanyika katika Msikiti wa Musalla Quds mjini Qom Iran, alisema: vitisho vya Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, zaidi ya kuonesha azma ya utekelezaji, ni dalili iliyo wazi ya kukwama kimkakati katika kambi ya adui.
Alisisitiza kuwa: katika mantiki ya Qur’ani Tukufu na Sunna za Mwenyezi Mungu, pale ambapo kambi ya batili inaposhindwa kuchukua hatua ya moja kwa moja na ya maamuzi, hukimbilia kelele, vitisho na vita vya kisaikolojia; kwa sababu njia za uwanja wa mapambano huwa na gharama kubwa na zisizotabirika. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 43 ya Sura Fatir:
“Na hila mbaya hazimzunguki mtu yeyote ila yule anayezifanya.”
Imam wa Ijumaa wa Qom alisema: Trump anajua kuwa kuingia vitani na Iran ni mwanzo wa njia isiyoweza kudhibitiwa mwisho wake; vita kama hivyo vitaliwasha eneo zima moto na kuathiri usalama wa nishati, uchumi wa dunia, pamoja na usalama wa kambi za kijeshi na washirika. Hofu na wasiwasi huu humtia adui woga na kumweka katika hali ya sintofahamu ya kimkakati.
Aliongeza kuwa: katika mantiki ya Sunna za Mwenyezi Mungu, kusitasita kwa kambi ya batili ni dalili ya kudhoofika kwa nguvu zake. Kama anavyosema Mwenyezi Mungu katika Aya ya 45 ya Sura Tawba:
“Ni wale tu wasiomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na ambao nyoyo zao zimejaa shaka, ndio huomba ruhusa [ya kukwepa jihadi]; nao katika shaka zao huendelea kusitasita.”
Khatibu wa Ijumaa wa Qom alieleza kuwa: pale hatua ya moja kwa moja inapokuwa hatari, basi hofu bandia hutumika kama silaha kuu; miongoni mwa athari zake ni kuathiri masoko, kuchochea taharuki katika jamii na kubadilisha mahesabu ya viongozi. Qur’ani Tukufu inafichua mbinu hii katika Aya ya 175 ya Sura Aal-Imran:
“Hakika huyo ni Shetani anayewatia hofu marafiki zake; basi msiwaogope wao, bali niogopeni Mimi ikiwa nyinyi ni Waumini.”
Alisisitiza kuwa: kutisha ni mbinu ya udhaifu, si dalili ya nguvu. Lengo la adui kutokana na vitisho hivi si vita, bali ni kusalimu amri bila vita. Adui kwa kukuza hofu anajaribu kuua dhamira ya mapambano miongoni mwa watu. Uzoefu umeonesha kuwa uwasilishaji wa wazi na thabiti wa ujumbe wa nguvu na msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu una athari kubwa zaidi katika mahesabu ya adui.
Ayatollah Saeedi aliendelea kusema: jukumu la kimataifa la jihadi ya kistaarabu ni kuendelea kuigharimu kambi ya batili bila kulazimika kuanzisha vita. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 60 ya Sura Anfal:
“Waandalieni nguvu kadiri muwezavyo na farasi wa kivita, ili kwa hayo mumtie hofu adui wa Mwenyezi Mungu na adui wenu, na wengine wasiokuwa wao msio wajua, lakini Mwenyezi Mungu anawajua.”
Aliongeza kuwa: maana ya kujiandaa kwa silaha si kwamba Waislamu wafanye uvamizi wa nchi nyingine, bali lengo ni kuwatisha maadui wa Mwenyezi Mungu na wenu—hasa makafiri na maadui wa Uislamu wasio na masikio ya kusikiliza haki.
Mwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi katika mji wa Qom alisema: maadui zenu wanaelewa tu lugha ya nguvu za kijeshi. Kwa njia hii, hata maadui msiowajua—ambao Mwenyezi Mungu anawajua—huwekwa mahali pao kiasi kwamba hata kufikiria kushambulia hawathubutu.
Akisisitiza umuhimu wa uimara wa ndani, mshikamano wa uongozi na kuimarisha uwezo wa kuzuia mashambulizi, alisema: ikiwa tunataka kufanikiwa katika njia hii, lazima tudumishe mshikamano wa ndani na wa utawala. Maelewano na sauti moja ya viongozi hutuma ujumbe wa uthabiti na nguvu ndani na nje ya nchi. Katika jihadi ya kistaarabu, “mshikamano wa uongozi” ni sehemu ya nguvu laini ya kuzuia.
Imam wa Ijumaa wa Qom amesema: Sauti nyingi zinazokinzana ndilo pengo ambalo adui analitafuta. Kama alivyoelekeza pia Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, hasa katika nyakati hizi ni lazima kulizingatia jambo hili. Kama Qur’ani Tukufu inavyosema katika Aya ya 4 ya Sura Saf:
“Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wale wanaopigana katika njia Yake wakiwa safu moja, kana kwamba wao ni jengo lililosukwa kwa chuma.”
Alikumbushia kuwa: Mwenyezi Mungu anawapenda wale wanaopigana katika safu moja kwa ajili Yake na kusimama kama jengo imara la chuma. Ikiwa maadui wa nchi za Kiislamu watawaona Waislamu wakiwa safu moja, hawatathubutu kuwashambulia.
Uvamizi wowote wa adui huimarisha mshikamano wa wananchi
Msimamizi wa Haram Takatifu ya Bibi Masuma (s.a.) alisema: uvamizi wowote wa adui husababisha mshikamano na umoja wa wananchi. Katika migogoro na fitna mbalimbali, tumeona kuwa adui anapoingilia kati, mshikamano wa taifa letu huongezeka. Taifa la Iran katika nyakati nyeti huwa na umoja na mshikamano mkubwa zaidi, na adui analijua hili. Ndio maana vitisho vya Trump si ishara ya nguvu, bali ni dalili ya kukwama kimkakati.
Imam wa Ijumaa wa Qom alisema: jihadi ya kistaarabu inatufundisha kuwa bila kuanzisha vita, lazima tudhoofishe azma ya adui na kuvuruga mahesabu yake. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imethibitisha kuwa, katika kujilinda hutenda kwa nguvu kamili na mamlaka kubwa, na taifa lote huungana kama ngumi moja nzito na kumpiga adui kinywani.
Akiwapongeza Waumini kutokana na maadhimisho ya kuzaliwa Imam Mahdi (a.s.), alisema: siku ya nusu ya Shaaban ni siku ya kuzaliwa kwa tumaini kuu la historia ya binadamu. Kama anavyosisitiza Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, matumaini ni chimbuko la harakati na maendeleo yote.
Khatibu wa Ijumaa wa Qom alibainisha kuwa: jukumu letu katika zama za ghaiba ya Imam wa Zama (a.s.) ni sawa na jukumu letu katika zama za uwepo wa Imam Maasum. Alisisitiza kuwa: jukumu kubwa zaidi la Mashia katika zama za ghaiba ni “kungoja kwa vitendo faraja ya dola ya kimataifa ya Imam wa Zama (a.s.)”. Faraja hii hutimia kwa kutekeleza maagizo ya Qur’ani, Mtume (s.a.w.) na Maimamu (a.s.).
Alisisitiza kuwa: kusubiri faraja si kauli mbiu ya kutamkwa tu, bali ni utamaduni unaohitaji nia thabiti na juhudi endelevu. Katika sherehe za nusu ya Shaaban, ni vyema kuzingatia zaidi upande wa maarifa na uelewa kuhusu Imam wa Zama (a.s.).
Askari wasiojulikana wa Imam wa Zama (a.s.) wana nafasi muhimu katika kuleta usalama
Mwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi mjini Qom, akitukuza Siku ya Askari Wasiojulikana wa Imam wa Zama (a.s.), alisema: taifa la Iran linajivunia kuwa na maelfu ya askari wasiojulikana wa Imam wa Zama (a.s.). Watumishi hawa wema wa Mwenyezi Mungu, katika hali zote—hasa katika nyakati ngumu za mfumo—kwa umakini na juhudi endelevu, hususan katika fitna za hivi karibuni, walivunja njama nzito zilizopangwa dhidi ya nchi. Askari hawa wa mfumo wa Mahdawiya wamekuwa na mchango mkubwa katika kuleta usalama na utulivu kwa wananchi.
Akiwapongeza Waislamu kwa kuzaliwa Ali Akbar (a.s.), alisema: jina la mama yake ni Laila. Miongoni mwa sifa za Ali Akbar (a.s.) ni kufanana kwake kwa kiwango cha juu kabisa na Mtume Muhammad (s.a.w.). Imam Hussein (a.s.) alisema kuhusu hilo:
“Alikuwa mtu anayefanana zaidi na Mtume wako katika umbile, tabia na maneno.” Na pia alisema pia: kila nilipohisi shauku ya kumuona babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), nilitazama uso wa Ali Akbar.
Msimamizi wa Haram Takatifu ya Bibi Masuma (s.a.) alisema: Ali Akbar (a.s.) ni mfano bora kwa vijana wetu, kwa sababu alikuwa amepambwa na maadili na fadhila njema.
Ayatollah Saeedi, katika khutba ya kwanza, alisema: Qur’ani Tukufu katika Aya ya 96 ya Sura A‘raf inaeleza uhusiano kati ya taqwa na baraka zake:
“Na lau kuwa watu wa miji wangeamini na wakamcha Mwenyezi Mungu, bila shaka tungeliwafungulia baraka kutoka mbinguni na ardhini.”
Imam wa Ijumaa wa Qom alisisitiza kuwa: Mwenyezi Mungu katika Aya hii anasema wazi kwamba athari za taqwa hazipo Akhera tu, bali pia zina matokeo katika maisha ya duniani.
Akiendelea na tafsiri ya Sura Fath, alisema: Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 13 ya Sura Fath:
“Na yeyote asiyemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, basi hakika tumewaandalia makafiri moto mkali.”
Imam wa Ijumaa wa Qom alibainisha kuwa: ukafiri una ngazi mbalimbali; si lazima mtu akane kuwepo kwa Mwenyezi Mungu au utume wa Mtume (s.a.w.w) ili ahesabiwe kafiri, bali hata kukanusha moja ya amri za Mwenyezi Mungu au Mtume Wake ni mfano wa “yeyote asiyemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.”
Aliongeza kuwa: mtu ambaye katika muundo wa itikadi na imani yake haitambui misingi mikuu ya imani, katika nyakati za misukosuko—hasa migogoro nyeti—huanguka kwenye matope ya upotovu; na huenda katika hali hiyo akamgeuzia Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w) mgongo, jambo linalompelekea kufru.
Khatibu wa Ijumaa wa Qom alisema: udini na imani ya mtu lazima ifikie kiwango ambacho anaiamini dini ya Mwenyezi Mungu na kuishi kwa misingi yake. Hapo ndipo mtu huwa Muumini. Watu wa aina hii hudumisha uhusiano wao na kiongozi na madhehebu, na katika misukosuko na majaribu hawapatwi na khofu.
Maoni yako